NENO LA MUNGU NI SILAHA

Friday, May 18, 2012

Imeandikwa mpingeni shetani naye atawakimbia. Na silaha pekee ya kumshinda ni upanga unaokata kuwili ambao ni neno la Mungu pekee. Yesu mwenyewe alitumia upanga huu wa neno la Mungu (Mathayo 4:4-11) tunatakiwa kunoa huu upanga kwa kusoma neno la Mungu mara kwa mara ili neno hili likae kwa wingi mioyoni mwetu. Na kila tunalopitia katika maisha yetu, iwe furaha au huzuni, lipo neno maalum ambalo limeandikwa katika bibilia tunatakiwa kusimamia. Na ukiweza kugundua siri hii kila litakalotokea katika maisha yako utakua hauna shaka bali utasema tu imeandikwa, kila jambo lina wakati wake, imeandikwa kwa kupigwa kwake tumepona, imeandikwa amebarikiwa mtu yule amtegemeaye Bwana nk.


Wengi tunatumia nguvu nyingi sana kumpinga shetani wakati yeye ni kijitu kidogo sana ambacho ukitumia silaha ya neno la Mungu tu huna haja ya kujichosha badala yake hizo nguvu zitumie katika kumsifu na kumwabudu Mungu ambaye anakaa katikati ya sifa!


Tuangalie mfano wa Yesu alipojaribiwa, alikua na uwezo wa kumtandika shetani makofi na kumharibu kabisa, lakini aliona hana sababu ya kujichosha wakati tayari Mungu ameweka upanga maalum wa kumuadhibu shetani ambao ni neno la Mungu pekee. Ndio maana kila Yesu alipojaribiwa alitumia neno "imeandikwa" mwisho wa siku shetani alimkimbia. Mungu akubariki wewe uliyesoma ujumbe huu!

0 comments:

Post a Comment