TAMBUA KUISHI NDANI YA KUSUDI LA MUNGU KATIKA MAJIRA NA NYAKATI UNAZOPITIA

Sunday, January 6, 2013

Katika kitabu cha mhubiri 3:1-8 inasema, Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu......
Maana yake ni kwamba, kila mtu kwa wakati huu anapita katika majira fulani ambapo ndani ya hayo majira liko kusudi maalum la Mungu kukupitisha katika majira hayo. Yawezekana unacheka au unafuraha kwa wakati huu, lakini kusudi la Mungu si ufurahi tu alafu basi, hapana, lipo kusudi, ambalo Mungu anataka ufanye kutokana na furaha uliyonayo, labda kucheka huko na kufurahi huko Mungu anataka utumie muda huo kufariji waliao na kuwaombea, au utumie muda huo kushuhudia matendo makuu ya Mungu kwa wengine. Yawezekana wakati huu unalia, kusudi la Mungu si ulie tu alafu basi, hapana, au si kwamba Mungu amekuacha ndo maana ukawa na huzuni na kuomboleza, lipo kusudi maalum la kiungu linalosababisha upite hapo, labda Mungu anataka ulie ili uondoe ule uchungu ambao umekua sumu ya kukumaliza kabla ya wakati wako, au Mungu anataka upendo wako kwake ukue zaidi na useme kwamba, "haijalishi hata machungu haya ninayopitia najua Mungu wangu aliye hai yupo pamoja nami na kamwe sitamuacha". Au yawezekana unapitia katika ugonjwa na maumivu makali sana, kiasi kwamba umekosa hamu ya kuendelea kuishi, nataka nikuambie, ndani ya ugonjwa huo na maumivu hayo lipo kusudi la kiungu ndani yake. Si kwamba Mungu anataka kukukomoa au anataka uteseke, hapana, huo sio mpango wa Mungu, acha kumlaumu na kujuta kwanini ulizaliwa, labda Mungu anakurudi kwa makosa yako na anachohitaji ni roho ya kutubu na kunyenyekea ifurike ndani yako, au labda anataka katika ugonjwa huo ulionao ajitukuze mwenyewe, "Yohana 9:3, Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake". Au Mungu anataka imani yako ikue na nguvu ya kuwekea wagonjwa mikono wapate afya ishuke juu yako.

Katika majira na nyakati zozote unazopitia kumbuka jambo moja, kwamba upendo wa Mungu kwetu ni mkuu sana na ndio maana akamtuma mwanae wa pekee Yesu Kristo ili aje kuukomboa ulimwengu katika dhambi na kila mateso na shida, na kutuweka huru mbali na kuonewa. Na kwamba Mungu haoni hasira upesi, ni mwepesi wa kusamehe hivyo basi hawezi kukupitisha katika majira fulani kukukomoa au basi tu, lazima ana sababu maalum iliyo sahihi kabisa, yenye faida kwako na kwa familia yako.

Unachotakiwa kufanya, badala ya kulaumu au kukata tamaa au kutumia wakati uliopo kinyume na kusudi la Mungu, unatakiwa kuutafuta uso wa Mungu zaidi na zaidi ili aweze kukuonyesha kusudi lake la kukupitisha katika majira na nyakati hizo. Tukiangalia habari ya Ayubu mtumishi wa Mungu Ayubu 42:5, Nilikua nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio yako; Bali sasa jicho langu linakuona. Hii inamaanisha kwamba kama Ayoub angeenda kinyume na kusudi la Mungu asingeyaona matendo makuu ya Mungu kwa macho yake, angeishia kusikia tu kwa wengine na angekufa, lakini kwakuwa alijua kwamba Mungu anampenda, aliamini ipo siku maombi yake yatajibiwa na machozi yake yatafutwa na Mungu. Nikuambie jambo moja, kinachoharibu kusudi la Mungu kutimia katika majira na nyakati tunazopitia ni kuenda au kuishi nje ya kusudi la Mungu. Bwana Yesu atusaidie tuweze kuishi ndani ya kusudi la Mungu katika majira na nyakati tunazopitia.

3 comments:

Unknown said...

Nimefurahi sana kuona mafundisho haya kwani yamenikumbusha Mafundisho ya Pastor Rick W. Barikiwa sana na Mungu

Unknown said...

Amen, Mungu akubariki pia kwa kutembelea blog hii@Fank

Mdee Junior said...

Glory to God, keep it.

Post a Comment